Mahamat Kamoun |
Muungano wa Seleka katika Jamhuri ya Afrika ya Kati umepinga uteuzi wa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo na kukataa kushiriki katika serikali ijayo. Mahamat Kamoum aliteuliwa hivi karibuni na Rais Catherine Samba-Panza kuwa Waziri Mkuu mpya wa serikali ya mpito ya nchi hiyo. Uteuzi wa Mahamat Kamoun ambaye ni Waziri Mkuu wa kwanza Mwislamu katika historia ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, ulitarajiwa kupunguza mivutano katika nchi hiyo.
Inaonekana hali haijawa kama ilivyotarajiwa, kwani masaa machache tu baada ya kutangazwa uteuzi wake, Muungano wa Seleka umetoa taarifa inayosisitiza kususia kushiriki katika serikali ijayo.
Rais Catherine Samba-Panza |
Fauka ya hayo, katika kipindi cha utawala wa Rais Francois Bozize, Kamoun alikuwa na wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa Hazina. Kamoun ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu baada ya kujiuzulu Andre Nzapayeke aliyekuwa akishikilia wadhifa huo. Nzapayeke na serikali yake, wamejiuzulu ili kupisha utekelezwaji wa hati ya makubaliano ya kusukuma mbele gurudumu la serikali ya mpito; makubaliano ambayo yalitiwa saini hivi karibuni huko Congo Brazzaville.
Makundi hasimu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, mwishoni mwa mwezi uliopita yalitia saini hati ya makubaliano ya amani. Pamoja na hayo, mapungufu yaliyoko katika hati ya makubaliano hayo kwa upande mmoja na kutofungamana na hati hiyo sambamba na kuweko hitilafu za ndani kwa upande wa pili, ni mambo yaliyopelekea kukiukwa usitishaji mapigano. Hivi sasa hitilafu kati ya pande mbili katika nchi hiyo zimeshika kasi zaidi. Inaonekana kutiwa saini makubaliano hayo kumeongeza hitilafu za miongoni mwa makundi hasimu. Ijumaa iliyopita mirengo mbalimbali ndani ya kundi la Kikristo la Anti-Balaka iligeukana na kuanza kupigana. Kushadidi mapigano hayo kumesababisha raia wengi kujeruhiwa na maelfu ya wengine kuyakimbia makazi yao.
Baadhi ya viongozi wa Seleka wametangaza wazi kwambva, wanapinga makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni huko Brazzaville. Mgawanyiko ndani ya kundi la Seleka umekuwa mkubwa kiasi kwamba, baadhi ya weledi wa mambo wanaona si jambo lililo mbali kuona likiibuka kundi jingine na kujitenga. Si hayo tu, mapigano baina ya wapiganaji wa Seleka na Anti-Balaka yameendelea kushuhudiwa licha ya pande mbili kutia saini hatia ya makubaliano ya amani.
wanajeshi katika doria |
No comments:
Post a Comment