Thursday, 25 September 2014

WAKAZI TABORA KUISULUBU CCM 2015


BAADHI ya wakazi mkoani hapa, wamesema kutokana na kuporwa viwanja na mashamba yao na Halmashauri ya Manispaa, watakihukumu chama tawala (CCM), kwenye uchaguzi mkuu mwakani kwa kuhamasishana na ndugu zao kukiangusha mkoani hapa.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wananchi zaidi ya 380 kutoka Kata za Malolo na Ipuli, walisema wameporwa maeneo yao ambayo walikuwa wakiyatumia kwa kuyaendeleza miaka mingi.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa kamati ya migogoro ya ardhi na mashamba Kata ya Malolo, Robert Jilala, alisema migogoro ya ardhi ilianza mwaka 2011 baada ya watumishi wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji Halmashauri ya Manispaa Tabora, kufika kwenye maeneo yao na kuwataka kusitisha kazi walizokuwa wanafanya.

Jilala, alisema walikuwa wakiyaendeleza maeneo yao kwa kulima mazao, ujenzi wa nyumba na walijulishwa maeneo hayo yatapimwa ili kuendeleza mji na wao watalipwa fidia.

Alisema watumishi wa Idara ya Ardhi walipomaliza kupima maeneo yao, walibadilishiwa lugha kwa kuelezwa upimaji uliofanyika ni mradi wa Manispaa, hivyo kila mwananchi mwenye eneo ama shamba atalipwa fidia ya fedha.
Alifafanua kuwa walijulishwa na watu wa ardhi kuwa, kila mita moja ya mraba watalipwa sh 150.

Jilala, alisema walipoomba wapimiwe ili wakabidhiwe maeneo yao walielezwa watalazimka kuyanunua kwa kati ya sh 2,000 hadi sh 2,800 kwa mita moja za mraba, hali ambayo iliwashangazwa na kuona haki yao inaporwa.
Aidha, mkazi mwingine wa Kata ya Ng`ambo, Said Juma, alisema alikuwa na ekari moja eneo la Mbirani, lakini ameambulia hundi ya sh 108,000 ambayo amelipwa mwaka 2013 kupitia benki ya NMB huku baadhi ya wenzake wakilipwa sh 50,000 na sh 80,000 kupitia hundi zao.

Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mpera Kata ya Ipuli, Aziz Kitamanwa, alisema binafsi amedhulumiwa kwa kulipwa hundi ya sh 105,000 ambazo zimelipwa kutokana na eneo lake la zaidi ya ekari moja.
Wananchi hao, wametishia kuishughulikia CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao kutokana na dhuluma waliyofanyiwa.HABARI NA   PRISCA  MUSHI

yeye ni mgeni ana mwezi mmoja Tabora hivyo hajui chochote. 

No comments:

Post a Comment