Dodoma. Wenyeviti wa Kamati za Bunge wametabiri mvutano mkali bungeni wakati wa kuwasilishwa kwa maoni ya kamati zote kuhusu Rasimu ya Katiba.
Wakizungumza jana baadhi ya wenyeviti walikiri kuwa katika kamati zao kulikuwa na mvutano mkali, jambo linaloashirikia kutakuwa na hali ngumu hata kwenye Bunge
.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Nne, Christopher Ole Sendeka alisema mjadala katika kamati yake ubishani ulikuwa ni mkali ambao wengi hawakutarajia.
Ole Sendeka alisema kwa picha iliyoonyeshwa katika kamati, hali itakuwa ngumu zaidi watakapoingia bungeni kwa kuwa kila mtu asingependa kuona mambo yanapita kwa kuburuzwa.
Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo yanaibua upinzani mkali kuwa ni muundo wa bunge la Muungano, ardhi na suala la uraia pacha.
“Hayo mambo yatakuwa ni magumu hata ndani ya Bunge. Suala la uraia pacha litakuwa ni gumzo kubwa, lakini pia muundo wa bunge unaweza kutuvutia muda katika mjadala wake,” alisema Sendeka.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Kamati Namba Tatu, Dk Francis Kasabubu alitaja ardhi ndiyo suala linalotarajia kuwa na upinzani mkali.
Dk Kasabubu alisema upinzani utakuwa ni mkali kutoka kwa wajumbe wengi lakini akasema hiyo ndiyo afya ya Katiba inayotarajiwa.
“Kupingana ndiyo msingi wa kupata Katiba bora. Haiwezekani watu wakawa kimya na kusikiliza wengine kama wafanyavyo walimu, hiyo haitakuwa Katiba,” alisema Kasabubu.
Makamu mwenyekiti wa Kamati Namba 11, Hamadi Yusufu Masauni alisema jambo pekee analotarajia kuwa litasumbua ni Muundo wa Bunge.
Alisema kuwa unapotajwa muundo wa bunge ndipo unapotajwa mfumo wa Muungano ambao umekuwa ni kero ya muda mrefu.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Ummi Mwalimu alitaja jambo pekee linalosumbua kuwa ni Sura ya Nne ambayo ni suala la fedha za pamoja.
HABARI NA ABDUL KARIM
HABARI NA ABDUL KARIM
No comments:
Post a Comment