Wednesday, 6 August 2014

Del Bosque atoa dukuduku la moyoni baada ya kustaafu kwa Xavi


 NA ELLEN BAMPALE
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Hispania Vicente del Bosque González, ameonyesha kusikitishwa na hatua iliyochukuliwa na kiungo wa FC Barcelona, Xavi Hernández Creus ya kutangaza kustahafu kuitumikiwa timu ya taifa.
Del Bosque, ambaye alikiongoza kikosi cha Hispania kutwaa ubingwa wa kombe la dunia mwaka 2010 huko nchini Afrika kusini kisha kombe la Ulaya mwaka 2012, amesema kuondoka kwa Xavi kwenye kikosi chake anaamini kumeacha pengo ambalo katu hatoweza kuliziba.
Amesema uhalisia wa mchezo wa soka ambao umekuwa ukionekana siku zote, unampa wakati mgumu wa kuamini kama ataweza kumpata mchezaji kama Xavi, kutokana na kuamini kiungo huyo mwenye umri wa miaka 34 alikuwa na uwezo wa kipekee wa kucheza soka kwa kuisaidia La Roja kutimiza malengo yake.
Hata hivyo mzee huyo mwenye umri wa miaka 63, amemtakia kila la kheri Xavi katika majukumu ya kuitumikia klabu yake ya FC Barcelona ambayo ina mikakati ya kutaka kurejesha heshima ya kutwaa mataji baada ya msimu uliopita kutoka kapa.
Xavi, ataendelea kukumbukwa katika majukumu yake alipokuwa na timu ya taifa ya Hispania tangu mwaka 2000, ambapo alionekana kuisaida sana safu ya kiungo katika upande wa ushambuliaji na mara kadhaa alionekana kutoa pasi za mwisho ambazo ziliiwezesha La Roja kutimiza malengo ya kupata ushindi.
Kumbu kumbu kubwa ambayo itaendelea kubaki kwa mashabiki wa soka nchini Hispania na pengine ulimwengu mzima, ni pasi ya mwisho ya kiungo huyo aliyoitoa wakati wa fainali za barani Ulaya za mwaka 2008 ambayo iliiwezesha timu ya taifa ya Hispania kutwaa ubingwa wa bara hilo, kufuatia bao pekee lililofungwa na mshambuliaji wa klabu ya Chelsea Fernando José Torres Sanz dhidi ya timu ya taifa ya Ujerumani.

No comments:

Post a Comment