Na STANLEY LEMA
0759 224505
Rais mpya wa Simba sc, Evans Elieza Aveva
WEKUNDU wa Msimbazi Simba juni 29 mwaka huu wamefanikiwa kupata viongozi wapya watakaoendesha gurudumu kwa miaka minne ijayo.
Hongera Evans Elieza Aveva kwa kuchaguliwa kwa kishindo kuwa rais wa kwanza wa Simba kwa kumbwaga kwa mbali mpinzani wako, Andrew Peter Tupa.
Pia Geofrey Nyange Kaburu hongera kwa kurudi kwa kishindao katika uongozi wa klabu ya Simba, safari hii `baba`! unaitwa Makamu wa Rais na sio makamu mwenyekiti kama siku zile unajiuzulu.
Pia niwape hongera Iddi Kajuna, Said Tully, Collins Frisch, Ally Suru Jasmine Badour kwa kuchaguliwa katika nafasi za wajumbe wa kamati ya utendaji.
Uchaguzi wa Simba sc ulikumbwa na mizengwe mingi, lakini mwisho wa siku ulimalizika salama.
Evans Aveva tangu uchaguliwe kuwa rais wa Simba, sijawahi kukueleza lolote, lakini leo hii nimejisikia kukuambia mambo machache baada ya kuitafakari Simba ya sasa.
Hakuna ubishi, kwa miaka miwili mitatu, Simba imekuwa ikiwapa machungu mashabiki wake kutokana na matokeo mabaya ya uwanjani ambayo imekuwa ikiyapata.
Simba imepita katika wakati mgumu kiuongozi. Migogoro ya ndani kwa ndani imeitafuna kwa muda mrefu. Uelewano baina ya viongozi haukuwepo na ndio maana mara kadhaa tulisikia kupinduana.
Makamu wa Rais wa klabu ya Simba sc, Geofrey Nyange `Kaburu` naye ana wajibu wa kuisaidia Simba kuwa mpya.
Hakika mambo yale hayakuwa na maana katika ustawi wa soka la Simba na Tanzania kwa ujumla.
Simba ni klabu kongwe yenye mashabiki wengi. Wachache kuiharibu ni kuumiza mioyo ya mamilioni ya watu wengi walioiweka klabu hiyo kwenye roho zao.
Aveva umeingia katika wakati mgumu ambao Simba ipo katika mpasuko ambao ulisababishwa na uongozi wa Ismail Aden Rage na baadaye uchaguzi uliokupa ushindi wa kishindo dhidi ya Tupa.
Nafahamu kulikuwa na kambi mbalimbali wakati wa uongozi, hususani ile ya Michael Richard Wambura aliyetabiriwa kuwa mpinzani wako mkubwa, lakini alienguliwa na kamati ya ucghaguzi chini ya mwenyekiti, Wakili Damas Daniel Ndumbaro.
Hizi kambi ni sumu katika uongozi wako, hivyo ukiwa kiongozi wa juu zaidi katika klabu ya Simba, unatakiwa kupigana kuzivunja kabisa.
Aveva nakusisitiza ujitahidi kuvunja makundi hayo kwasababu yatakufanya ushindwe kufikia malengo yako. Hakuna haja ya kuwachukia wala kuwafikiria vibaya waliokuwa wakikupinga hadharani.
Moja ya mambo yanayowaathiri wanasiasa wengi ni kuendeleza chuki baada ya uchaguzi. Kama mtu alikuwa anakupinga wakati unamwaga sera, haimaanishi ni adui yako.
Mambo ya demokrasia ndivyo yalivyo. Kupinga na kuunga mkono ni haki ya kila mtu. Haiwezekani na haitawezekana uungwe mkono na kila mtu. Basi watu hao watakuwa hawafikirii vizuri.
Nilikusikia kwa mara ya kwanza ukizungumza baada ya kuchaguliwa. Uliweka wazi dhamira yako ya kuvunja makundi. Nafahamu wakati wa uchaguzi kuna watu walitukanana na kusemana maisha binafsi na kusababisha chuki za nje ya mpira sababu ikiwa ni wagombea ukiwemo wewe.
Lakini haya yote yanatakiwa kufutwa ili maisha yaanze kwenda barabara. Aveva wewe ndiye mwenye dhamana ya kuwezesha hili na unatakiwa kuwa na washauri wazuri juu ya kumaliza tofauti hizi.
Nategemea uheshimu sera watu wote waliokuwa wanaomba nafasi, Kuna faida kubwa ya kuongeza ya wenzako kichwani mwako. Naamini Tupa alikuwa na sera nzuri, lakini wewe umepata nafasi. Mawazo yake usiyapuuze.
Hata Wambura alikuwa na mawazo mazuri kwa klabu, japokuwa bahati mbaya wengi walisahau kufikiria mawazo hayo kutokana na matatizo aliyokuwa nayo. Lakini jaribu kutafakari mawazo yake pia.
Aveva nitafurahi sana kama utafanya yafuatayo katika uongozi wako:
Mosi; ufanikiwe kujenga uwanja wa klabu. Kwa muda mrefu Simba haina uwanja. Hii ni historia mbaya kwa klabu kubwa kama hii. Ndani ya miaka minne unao uwezo wa kuunganisha nguvu ya wanasimba wote na kufanikiwa kujenga uwanja wa kisasa.
Najua wapo watu wengi nyuma yako na wana uwezo mkubwa wa kifedha. Kwa kutumia urafiki na nguvu ya uongozi, jaribu kuwashawishi ili dhamira yako ya uwanja itimie. Umekuwa rais wa kwanza wa Simba na ukifanikiwa kujenga uwanja, utakuwa Rais wa kwanza kujenga uwanja wa Simba. Utaingia katika historia ya klabu na kuwa miongini mwa watu wenye heshima milele.
Naamini zipo jitihada zinazoendelea huko Bunju katika uwanja wenu, lakini Aveva na wenzako mnao uwezo wa kufanikisha zaidi.
Ukijenga uwanja katika kipindi chako cha miaka minne, nitakuwa na la kusema mwaka 2018.
Pili; Aveva achana na mfumo wa kuifanya Simba klabu ya kuifunga Yanga tu. Ni kwa muda mrefu sasa, viongozi na makocha wamekuwa wakitolewa `Kafara` kila wanapofungwa na mtani.
Hili lipo hata kwa Yanga. Ukiwa kocha wa Yanga, kufungwa na Simba ni hatari katika kazi yako, vivyo hivyo kwa Simba kufungwa na Yanga ni majanga.
Mserbia, Milovan Circovic aliwahi kuifunga Yanga mabao 5-0, alionekana kocha bora zaidi japokuwa aliachishwa kazi. Mfaransa Patric Liewig alionekana kuwa kocha bora, lakini matokeo aliyoyapa katika mechi za Yanga, yalikuwa na nguvu ya kumuondoa katika kazi yake.
Hata Abdallah Kibadeni sare ya 3-3 ilichangia kumfuta kazi Msimbazi. Dravko Logarusic aliifunga Yanga mabao 3-1 kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe mwezi desemba mwaka jana na katika mechi ya marudiano ya ligi kuu soka Tanzania bara alitoka sare ya 1-1.
Matokeo haya kwa kiasi kikubwa yalichangia kuendelea na kazi yake Simba na kupewa mkataba wa miaka miwili na uongozi wa Aden Rage.
Ernie Brandts aliwapa Yanga ubingwa, lakini kipigo cha Nani Mtani Jembe kilifungua balaa kwake kwasababu alionekana kuwa na kikosi bora na akashutumiwa kuwa timu imeshuka kiwango. Lakini ukweli ni kufungwa na Simba.
Aveva wakati huu si muda wa Simba kuiendea Yanga Zanzibar, halafu mechi nyingine inafungwa. Ni muda muafaka wa kuifanya Simba kuwa klabu ya kisasa na ya ushindani, Tanzania na nje ya Tanzania.
Tengeneza mkakati wa muda mrefu. Tengeneza soka la vijana na kuwaamini makocha ili watekeleze mipango yao.
Najua umechaguliwa kwa kura, hivyo utaogopa kuwaumiza wapiga kura wako na kutaka kufanya mambo kama watakavyo, lakini kumbuka mpira una misingi yake. Kuwa na mipango na itekeleze kwa ueledi mkubwa.
Tatu; Angalia namna ya kuuza jezi. Kuna mamilioni ya mashabiki wa Simba sc nchi nzima, nembo yenu ni kubwa. Kuna uwezekano mkubwa wa kuingiza pesa ndefu kupitia jezi zenu. Katika uongozi wako, fungua maduka ya jezi na vifaa vya Simba. Weka usimamizi mzuri, nakuhakikishia, utaitoa Simba hapa ilipo.
Nne; dhibiti uwizi wa mapato ya Simba. Kuna `wahuni` ambao miaka na miaka, Simba ni kitega uchumi kwako. Tafuta njia ya kuwasaka watu hawa na kuwabaini. Kama utazuia upotevu wa mapato, utaisaidia Simba kwa kiasi kikubwa. Utaitoa mikononi mwa watu wachache na kuwa timu ya kujitegemea.
Tano; tafuta washauri wazuri katika maamuzi yako. Tumeshuhudia viongozi wa ngazi za juu katika vyama vya mpira wakifanya maamuzi ya kukurupuka. Wengine wanalala na kuamka na maamuzi. Epuka usanii wa namna hiyo. Tafuta washauri wazuri kwa ajili ya manufaa ya klabu.
Yapo mengi ya kukwambia Aveva, Rais Mteule wa Simba. Siku utakayokabidhiwa kijiti rasmi na mhe. Ismail Aden Rage, nitakueleza kitu.
Vinginevyo, niwapongeze sana wana Simba kwa kufanikisha uchaguzi wenu.
No comments:
Post a Comment