Monday, 10 March 2014

Dk Slaa awaonya wanachama


Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo nchini (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, amewaonya baadhi ya wanachama wanaochafuana kwenye chama hicho waache mara moja vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
 
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Dk. Slaa amesema, kutangaza nia siyo dhambi ni haki ya mwanachama bila kuwapo kwa migogoro ila anapaswa afuate kanuni za chama.
 
Hata hivyo, Dk. Slaa amekanusha kuwapo kwa mpasuko ndani ya chama Jimbo la Songea mjini ambapo alisema yeye kama katibu mkuu bado hajapata malalamiko rasmi ya wanachama kugombana ingawa amekemea wanachama kuchafuana na kuzushiana uongo.
 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kanda  Kusini, Matiko Matale, alipohojiwa alisema kuwa taarifa ya Mwenyekiti wa Chama hicho mkoa kutangaza nia ya kugombea ubunge jimbo la Songea mjini alipata ila hakufuata utaratibu na wala hakupata baraka toka ndani ya chama.
 
Alisema kwa sasa anajiandaa kuitisha kikao cha kamati ya utendaji cha kanda ili kujadili mambo mbalimbali yakiwamo ya chaguzi  kwani ametangaza nia mapema.
 
Naye mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chadema Taifa, Edson Mbogoro, amewaambia waandishi wa habari kuwa kutangaza nia siyo dhambi ila yeye binafsi anasubiri mchakato  na taratibu za chama zinavyoagiza.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho mkoa Joseph Fuime hakuweza kupatikana kuzungumzia tuhuma hizo kwani kila alipopigiwa simu zake zote za mkononi zilikuwa zimezimwa.

No comments:

Post a Comment